Sina jinsi. Nguzo ya maisha yangu ni historia ya maisha yangu. Historia ya maisha yangu ni urithi wa watu waliojifunza kusema hapana kwa ndiyo nyingi – waliojitolea vitu vingi katika maisha yao kunifikisha hapa nilipo leo – walionifundisha falsafa ya kushindwa si hiari. Siri ya mafanikio yangu ni kujitahidi kwa kadiri ya uwezo wangu wote; au 'pushing the envelope' kwa lugha ya kigeni.
Ukiwaza kitu kwa dakika moja na sekunde nane – huu ni utafiti wangu tu – hicho kitu kitaanza kujiumba kwa ajili yako sehemu fulani ulimwenguni. Ukiamini kwa kiasi cha kutosha kwamba umekipata, utakipata. Haijalishi kama una elimu au huna. Hiyo ndiyo siri kubwa zaidi ya utajiri kuliko zote duniani – MAWAZO YAKO.
Kama Shetani anatumia elimu kutawala dunia kama vile Mungu anavyotumia elimu kutawala dunia, nani alisema kuwa baadhi ya wasanii wa ‘Bongo Movie’ na ‘Bongo Flava’ ni wanachama wa chama cha siri cha kusaidiana cha wajenzi huru? Je, wana elimu? Jibu unalo.